0
Miaka takribani saba iliyopita kwenye mtaa fulani hapa Njombe katika usiku wa giza zito uliofunikwa na baridi kali iliyochangamana na ukungu, wapo vijana kadhaa wamelala chini ya mitaro, wamesogeleana karibu ili angalau wapate joto katika miili yao. Mashuka yao ni maboksi yaliyotolewa vitu vya thamani na kutupwa jalalani.
Kati ya vijana hawa ambao wamelala chini ya moja ya mitaro ya mji huu wa Njombe yupo kijana aitwaye John Mwingira ambaye kabla ya miaka saba iliyopita alikuwa akiishi nyumbani kwao Ifakara, wilayani Kilombero mkoani Morogoro.
Huko alikuwa akiishi na wazazi wake wote wawili, lakini baadaye wazazi wake waliachana kufuatia kutokuwepo maelewano baina yao. Baba yake akahamia Njombe na mama yake akabakia Ifakara.
“Baada ya wazazi wangu kuachana maisha yalikuwa magumu pale nyumbani Ifakara hivyo mama akanishauri nimfuate baba hapa Njombe, nilifika Njombe na kuonana na baba yangu ambaye tayari alikuwa ameoa mke mwingine”, anasema John.
Maisha ya John na mama yake mpya hayakwenda vizuri kwani mama huyo hakumpenda. Chuki, kazi nyingi na kugombezwa zikamfanya baba mzazi wa John kutafuta chumba maeneo ya Mgendera na kumpangishia mwanaye.
Kama walivyo wazazi wengine wasiojali, baba yake John akaanza kumtelekeza John taratibu na hatimaye mawasiliano kati yao yakafa kabisa. Shida nyingi zikamfika John na moja ya shida hizo ni chakula na pango la nyumba.
“Nakumbuka baada ya baba kunitelekeza maisha yakabana zaidi, hapo ikabidi niwe naelekea mjini kutafuta kazi ambazo pia sikupata hali iliyopelekea kufukuzwa katika chumba alichokuwa amenipangia baba huku mwenye nyumba akaninyanganya kitanda ili kufidia kodi yake.”
Baada ya kuwa amefukuzwa katika chumba alichokuwa akiishi John aliamua kuingia mtaani, akawa mmoja wa watoto wa mtaani, huko maisha mapya ya ubabe, utumiaji madawa ya kulevya, Ulawiti, kesi za kusingiziwa wizi, kuomba kwa wapiti njia, na kufukua jalalani akitafuta chakula na vyuma chakavu ikawa sehemu yake ya maisha.
“Maisha ya mtaani yalikuwa machungu zaidi ya kifo unachokijua..kila siku mimi na watoto wengine walionikaribisha mtaani tulizurura kila kona tukitafuta chakula, mavazi na malazi…nilijawa hofu sana, sikuwa na raha na wasiwasi mwingi ulizunguka maisha yangu..lakini ningefanya nini!? Hapana, sikuwa na namna ya kufanya…nilijipa moyo nikajikaza kiume na kuendelea na maisha” anaeleza John.

Mitazamo hasi ya jamii kuhusu watoto wa mitaani mara nyingi imekuwa chachu ya kufanya maisha ya watoto hawa kuwa magumu na hivyo kuwalazimisha kufanya matukio mengine ambayo katika maisha yao hawakuwahi kufikiria kuyafanya.
John anabainisha wazi kwamba ipo sehemu ya jamii inawaona watoto wa mtaani kama nuksi, vibaka, wabakaji. Na kwa sababu hiyo wameamua kuwatega mgongo.
“Kwa kuwa jamii na serikali imetutenga hii inakuwa fursa ya wakora wengine kututendea watoto wa mitaani matendo maovu wayatakayo, siku moja tukiwa tumelala katika moja ya mitaa ya Njombe tulivamiwa na kundi la watu wanaotuzidi umri wanaonekana kuwa na maisha safi, wakawashika watoto watatu kati yetu mimi na baadhi ya wenzangu tukakimbia, ajabu wale watu waliwalawiti wale watoto wenzangu, zingatia kuwa umri wa watoto wale ulikuwa kati ya miaka 10 mpaka 13.”
kuhusu kupewa misaada na jamii ya watu waishio Njombe John anasema,
“..katika kipindi nilichokuwa nikiishi mtaani wapo wachache waliotusaidia sisi watoto wa mtaani, lakini kibaya zaidi wale ambao mnawaita matajiri, wenye pesa zao na magari ya kifahari hapa Njombe na wanaoishi kwenye nyumba zilizondani ya kuta za gharama kubwa hakuna hata mmoja kati ya hao aliyewahi kutusaidia” aliongeza.
Badala yake John aliueleza ukurasa huu kuwa msaada mkubwa waliupata kutoka kwa masikini na watu wenye kipato cha kawaida.
Nilipomuuliza kuhusu wapi alipo baba yake, hivi ndivyo alivyosema John,
“Baada ya kukaa muda mrefu bila ya kuonana ama kuwasiliana na baba yangu baadaye nilipata taarifa kuwa alifariki dunia siku nyingi, natamani ningeweza kumuona japo kwa mara ya mwisho ama kufahamu wapi kaburi lake lilipo niende kulitembelea lakini haijawa hivyo, kwa hili nasikitika sana.”
John kwa sasa anaishi katika kituo cha kulea watoto waishio katika mazingira magumu cha ‘Compasion’ cha Airport mjini Njombe, anakiri na kushukuru kufika hapo kwani kituo kinamsomesha kwa gharama zake. Hivi sasa yupo kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Mpechi.
Kijana huyu ni mjuzi pia wa masuala ya umeme pamoja na utengenezaji madishi ya Luninga, kupitia kipawa alichonacho unaweza kumpa ajira ambayo mwisho wa siku ikampatia kipato na hivyo kumpa maisha bora.

Chapisha Maoni

 
Top